Zanzibar |
VITAMBULISHO VYA UZANZIBARI VYAZUA BALAA
Vyama vya upinzani Zanzibar, vimeshauri Sheria ya Uzanzibari ya Ukaazi ifanyiwe marekebisho kabla ya utaratibu wa uandikishaji wapigakura unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Msimamo
huo wameutoa baada ya Mkuu wa Divisheni ya Uchaguzi Zanzibar, Idrisa Haji Jecha
kutangaza kuwa kazi ya uandishaji wapigakura wapya katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura litafanyika siku mbili kwa kila kituo baada ya kura ya maoni ya
Katiba Inayopendekezwa kufanyika Aprili 30.
Alisema
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeweka siku mbili za uandikishaji kwa kila
kituo kutokana na muda mdogo uliobakia kuelekea uchaguzi mkuu kutokana na mambo
mawili kufanyika kwa wakati mmoja.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib alisema kuwa sheria ya vitambulisho
vya Mzanzibari Mkaazi kuna umuhimu wa kufanyiwa marekebisho kabla ya
uandikishaji kuanza, kutokana na wananchi wengi kushindwa kumudu masharti ya
kupata vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi.
“Wapo
wananchi wengi hawana vyeti vya kuzaliwa na kumekuwapo na urasimu wa kupata
fomu kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa (Masheha), lazima sheria
irekebishwe kupunguza masharti ya kupata kitamburisho cha Uzanzibari
Ukaazi,”alisema.
Khatib
alisema pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010,
imeshindwa kuondoa tatizo la upatikanaji wa vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi
pamoja na vyeti vya kuzaliwa na kusababisha wananchi wengi kushindwa kupata
haki ya kuandikishwa kuwa wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura
visiwani humo.
“Pamoja
na Rais, Dk Shein (Dk Ali Mohamed Shein) kuonyesha utendaji mzuri, wasaidizi
wake wanamwangusha, wameshindwa kuondoa tatizo la upatikanaji wa vyeti vya
kuzaliwa pamoja na urasimu wa fomu za kuwawezesha wananchi kupata Uzanzibari
Ukaazi,” alisema Khatib.
Alisema
wakati umefika Baraza la Mawaziri kujadili sheria ya Uzanzibari Ukaazi na
kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria kabla ya Baraza la Wawakilishi
kuvunjwa baada ya kikao cha bajeti mwaka huu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omari Ali Shehe, alisema
kuwa utafiti uliofanywa na chama hicho umebaini kuna watu karibu 12,000
hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kutokana na kukosa
vyeti vya kuzaliwa na urasimu wa upatikanaji fomu za kuwawezesha kupata
vitambulisho vya Uzanzibari Ukaazi kutoka kwa Masheha.
“Muda
wa uandikishaji hautoshi na sheria inahitaji kuangaliwa upya kupunguza masharti
ya sifa za kupata kitambulisho cha Uzanzibari Ukaazi, ili wananchi wengi waweze
kupata haki ya kikatiba,” alisema Shehe.
Alisema
kuwa kuna wazee wana miaka 60 hadi 70 wamekwama kupata vitambulisho vya
Uzanzibari Ukaazi kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa pamoja na kuwa wanaishi
katika mtaa mmoja na Sheha, lakini bado wameshindwa kupewa fomu na kusajiliwa.
Shehe
alisema ili uweze kukamilisha taratibu za kupata cheti cha kuzaliwa, karibu
Sh35,000 zinahitajika kama gharama za ufuatiliaji, jambo ambalo limekuwa
likiwashinda wananchi wengi kutokana na matatizo ya umaskini.
Tweet