Humphrey Polepole |
Rasimu ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote kama wakienda kinyume na masilahi ya wananchi katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao, iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze kumwajibisha mpaka miaka mitano?
Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti haya.
1. Kupunguzwa kwa madaraka ya raisi
Wananchi walipendekeza madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe taasisi za kikatiba za kumshauri rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi walipendekeza pia baada ya rais kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa huyo Bunge limthibitishe.
Katiba
Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na imemwongezea Rais madaraka.
2. Kutenganisha mamlaka ya mihimili ya dola
Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na mamlaka zaidi kwa Bunge kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali. Pendekezo hili linaenda sambamba na kutenganisha Serikali na Bunge, hali ambayo iko sasa. Rasimu ya Warioba ililipa Bunge mamlaka zaidi kuisimamia Serikali na hata pale ambapo Bunge lingekataa bajeti au muswada mbaya wa Serikali mara kadhaa, rais asingeliweza kulivunja Bunge. Wananchi walisema sana mawaziri wasitokane na wabunge, ili wabunge wafanye kazi ya uwakilishi pekee na mawaziri watumie weledi wao kumsaidia rais kazi za Serikali.
Katiba
Inayopendekezwa imefuta masharti haya.
3. Kumwajibisha mbunge
Rasimu
ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha wabunge kwa kupiga
kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote kama wakienda kinyume na masilahi
ya wananchi katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi
wao, iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze
kumwajibisha mpaka miaka mitano?
Katiba
Inayopendekezwa imefuta masharti haya.
4. Vyanzo vya mapato vya kuaminika
Kuwapo
kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakavyogharimia
mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka 22 hadi 7 lilikuwa pendekezo
ambalo hata taasisi za Serikali zilipendekeza. Katiba Inayopendekezwa
imerudisha mapato ya Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977 na kwa kufanya hivyo
tumerudi kwenye mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa forodha,
ushuru wa bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na kuifanya
ishindwe kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na vivyo
hivyo kwa Tanganyika.
5.Muundo wa shirikisho lenye mamlaka kamili
Kwa
miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha ni muundo gani wa Muungano Jamhuri
yetu inao. Kitendawili hiki kimeelezwa na wengi akiwamo Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere. Rasimu ya Warioba iliweka kwa mara ya kwanza Muundo Jamhuri ya
Muungano kuwa ni wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili, nchi moja na yenye
Serikali tatu. Kilichoongezwa ni na Rasimu ya Warioba ilikuwa Bunge na Serikali
ya Tanganyika na siyo nchi ya Tanganyika kama ambavyo wengi wameaminishwa hivyo.
Katiba Inayopendekezwa imerejesha na kuudhoofisha zaidi muundo wa Serikali
mbili, kwa kuifanya Tanganyika au Tanzania Bara kuwa ndiyo Jamhuri ya Muungano
na Zanzibar kuwa na mamlaka zaidi kwa mambo yasiyo ya Muungano ikiwamo kujiunga
na jumuiya za kimataifa.
6. Kupunguza ukubwa wa Serikali
Wananchi
walionesha kutofurahishwa na ukubwa wa Serikali unaopelekea matumizi makubwa ya
fedha za walipa kodi. Walipendekeza uwapo wa Serikali ya Muungano iliyo imara,
yenye ufanisi na ndogo. Rasimu ya Warioba ilisema idadi ya mawaziri isizidi 15.
Katiba
Inayopendekezwa inasema mawaziri wasizidi 40, pendekezo hili halina uhalisia
kwa sababu Serikali ya Muungano itashughulika na mambo ya Muungano na mambo
yasiyo ya Muungano ya Tanganyika/ Tanzania Bara na kuifanya kuwa kubwa zaidi na
hivyo kuhitaji mawaziri zaidi ya 40, kiufupi pendekezo hili halitekelezeki.
7. Tume ya Uhusiano na Uratibu
Rasimu
ya Warioba ililenga kuhakikisha kunakuwapo uhusiano mzuri, mawasiliano na
uratibu wa serikali zote tatu chini ya Mamlaka ya Serikali ya Muungano na
kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu. Bunge Maalumu lilishindwa kuelewa mantiki
ya pendekezo hili na Katiba Inayopendekezwa imelivuruga kabisa, kutoka
pendekezo la Warioba la “Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali” hadi “Tume ya
Uratibu wa Mambo ya Muungano” katika Katiba Inayopendekezwa.
8.Kupunguza ukubwa wa Bunge
Wananchi
walizungumzia pia ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na gharama
zinazoambatana nalo na wakapendeza Bunge dogo na lenye ufanisi mkubwa. Warioba
alisema idadi ya wabunge isizidi 75, Bunge Maalumu likasema wabunge wasipungue
340 na wasizidi 390.
9. Ukomo wa vipindi vya ubunge
Wananchi
walizungumzia nafasi za ubunge kuhodhiwa na watu fulani kwa miaka nenda rudi na
wakapendekeza ifike mahali kuwe na ukomo ili kuleta uwakilishi mpana na
mabadiliko. Rasimu ya Warioba iliweka ukomo wa vipindi vya ubunge kuwa vitatu
na kuwa na ukomo wa miaka 15 kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Bunge Maalumu na
Katiba Inayopendekezwa wamefuta pendekezo hili.
10. Kuwapo kwa tunu za Taifa
Wananchi
walipendekeza uwapo wa tunu za Taifa katika Katiba, tunu hizi ni pamoja na utu,
uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa. Raia wa
Tanzania walikuwa na wajibu wa kuheshimu tunu hizi lakini Katiba
Inayopendekezwa imezifuta tunu hizi.
11. Maadili na miiko ya viongozi
Wananchi
walizungumza kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya jamii, watumishi na
viongozi wa umma, wengi wakisema Katiba iainishe maadili na miiko ya viongozi
wa umma ambayo kwayo tutawawajibisha. Katiba Inayopendekezwa imesema maadili na
miiko kwa viongozi (mathalan kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha
mgongano wa masilahi), isiwamo kwenye Katiba bali ikawekwe kwenye sheria.
12. Masharti yasiyoweza
kubadilishwa na Bunge
Rasimu
ya Warioba iliweka masharti ya kuzuia Bunge kubadili baadhi ya masharti
mahususi ya Katib, ibara ya 119 isipokuwa kwa ridhaa ya wananchi kupitia kura
ya maoni (mathalan malengo makuu ya Taifa, haki za binadamu n.k. Pia, bahati
mbaya tulisahau kuweka na Sura ya tatu juu ya maadili). Masharti yote ya Ibara
hii yamefutwa isipokuwa Muundo wa Muungano na Uwapo wa Jamhuri ya Muungano.
13. Kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi
Wananchi
walizungumza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itakuwa na jukumu
la kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano. Ilisisitizwa juu ya umuhimu
wa tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kwamba mwenyekiti wa tume na makamu
wake wathibitishwe na Bunge ili kuwapa uhalali wa kitaifa, pendekezo hili
limefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
14. Usawa wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume
Kuwapo
uwiano wa uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume ni lazima kwa
mazingira ya sasa. Uwiano kati ya wanawake na wanaume katika vyombo mbalimbali
vya dola hasa vile vya kutunga sheria limeendelea kuwa tatizo nchini na
lililokaa kwa muda mrefu.
Wananchi
na hasa wanawake na baadhi ya wanaume walipendekeza uwiano ulio sawa katika
kufikia fursa hasa ukizingatia wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa. Rasimu ya
Warioba ilipendekeza katika kila jimbo kutakuwa na wabunge wawili, wa kike na
wa kiume, Katiba Inayopendekezwa imefutilia mbali pendekezo hili muhimu
15. Kuanzishwa kwa mgombea huru
Haki
ya wananchi kushiriki shughuli za umma imekuwa ikizuiwa siku nyingi na kwamba
ushiriki katika shughuli za umma kama kiongozi wa kuchaguliwa inapaswa kuwa
haki ya msingi ya mwananchi yeyote yule. Rasimu ilitoa haki ya mgombea huru
bila vikwazo, Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti magumu ambayo hakuna mtu
anayeweza kuyatimiza kirahisi, kitendo hiki siyo sawa.
16. Msaada wa kisheria kwa wananchi
Wananchi
walieleza kutokuridhishwa kwao na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi
wenye uhitaji huo na wakapenda huduma ya msaada wa kisheria liwe suala la
kikatiba kwa mwananchi yeyote yule na serikali iwajibike kutoa huduma hiyo.
Katiba
Inayopendekezwa imesema wananchi hawatakuwa na haki ya kudai huduma hii kokote
nchini, hata mahakama hazitaweza kusikiliza mashauri ama Serikali imetoa haki
hii au haikutoa haki hii rejea Ibara ya 21.
17. Uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi
Rasimu
ya Warioba ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa uhuru,
bila woga, upendeleo wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na
sheria za nchi. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
18. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania
Tume
ya Warioba ilipendekeza kuwapo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi
wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya utumishi katika
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba Inayopendekezwa imefuta
masharti haya licha ya wapiganaji kupendekeza utaratibu wa kusimamia masilahi
yao kikatiba.
19. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
Kutakuwa
na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la kusimamia
utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika uajiri wa askari wa Jeshi la Polisi, Tume
ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni na misingi ya utumishi
iliyoainishwa katika Katiba hii