Dar
es Salaam. Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) na
ITV/ Radio One wamesaini makubaliano ya kuandaa midahalo ya wagombea wa urais
kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Akizungumza
baada ya kutia saini makubaliano hayo jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Udasa,
Profesa Kitila Mkumbo alisema katika nchi za kidemokrasia midahalo hufanikisha
uchaguzi ulio huru, haki na wazi.
Pia,
alisema midahalo hiyo hutoa fursa muhimu kwa wagombea kueleza falsafa, sera na
mikakati yao ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.
Hata
hivyo, Profesa Mkumbo alisema midahalo watakayoendesha haitaegemea chama
chochote na kwamba mgombea atakayekataa kushiriki hawamlazimishi.
“Hatutakuwa
na uwezo wa kumlazimisha mgombea, nchi hii ina historia ya wagombea kukimbia
midahalo,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema
muda rasmi wa kuanza kwa midahalo hiyo utatangazwa baadaye, wananchi wajue kuwa
kupitia matangazo hayo wapiga kura watajua weledi na umahiri wa wagombea na
vyama vyao.
“Tafiti
zinaonyesha kuwa midahalo ya wagombea urais ina nafasi ya kipekee katika
kuwawezesha wapiga kura kuamua mgombea gani wamchague,” alisema.
Alisema
kuwa vyama vyote vitakavyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na ambavyo
vitasimamisha wagombea wa urais vitaalikwa kushiriki katika midahalo hiyo.
Pia
wagombea wote watakaojitokeza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu
wataalikwa kushiriki mdahalo huo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile alisema
midahalo hiyo itaaminiwa na wananchi kwa sababu wanaoandaa hawagombei nafasi
yoyote katika uchaguzi huo.
Tweet