Tangu
mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika nyingi za kisiasa ndani ya vyama vya
siasa na Jumanne iliyopita CCM ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini Zanzibar na
kutoa maazimio yanayogusia mchakato huo lakini ikasita kutaja ratiba rasmi ya
mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati
hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya viongozi
wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini Dar es Salaam Januari 20, ukiwa na ajenda
mbalimbali kuhusu ushirikiano wao, likiwamo suala la kupata wagombea huku vikao
vya ndani ya vyama vikitarajiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne
akisema kutakuwa na ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo
huenda likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa
sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda
nyingine alizotaja ni mwongozo wa Ukawa, kura ya maoni ya Katiba, changamoto za
uandikishaji wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na tathmini ya Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka jana. Mbatia, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha
wanatafuta majibu ya changamoto zilizopo kwa sasa.
Kiongozi
huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila chama ndani ya Ukawa kupitia vikao
vyake kitateua majina ya wagombea ambao watashindanishwa ndani ya umoja huo,
akisema kabla ya Machi, jina la mgombea urais ndani ya chama chake litakuwa
limeshapendekezwa.
Awali,
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema vikao vya chama hicho
vinavyotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na ajenda ya uchaguzi
vitakavyojadili mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda yake inavyosema.
“Nadhani
vikao hivyo ndiyo vitaanza kujadili ajenda ya uchaguzi ujao. Tulishatoa nafasi
ya watu kujitokeza kwenye nafasi mbalimbali. Tukishapendekeza majina ya
wagombea kwa baadaye ndiyo tutawapeleka ili kuchambuliwa kwa pamoja na kamati
ya Ukawa.
“Mpaka
sasa kamati ya Ukawa inaendelea na kazi yake tangu Oktoba mwaka jana ila
inakuwa vigumu kwa wajumbe kujua kazi zote zinazofanywa na kamati hiyo kutokana
na msingi wa majukumu yake.”
Nyambabe
alisema kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi, ikijumuisha wajumbe wasiopungua
watatu kutoka kila chama ili kufanya tathimini, kuchambua na kuratibu shughuli
zote za uchaguzi.
Kuhusu
kupata mwongozo wa Ukawa, Nyambabe alisema: “Namna ya kupata mgombea, ilani
moja na mwelekeo, vinaweza kuonekana kuanzia Februari baada ya vyama kukaa
vikao vyake.”
Wakati
Nyambabe akisema hayo, kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari kuwa CUF
kimeshatangaza kumsimamisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwania urais, ambazo hata
hivyo, zimekanushwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Magdalena Sakaya.
Alisema
kikao cha hivi karibuni ndani ya chama hicho kilikuwa na ajenda ya kutathimini
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tu na hakukuwa na ajenda nyingine iliyojadiliwa.
“Bado hatujapendekeza jina lolote,” alisema Sakaya.
Hata
hivyo, Sakaya alisema kikao kijacho cha wenyeviti wa Ukawa hakitakuwa na
mamlaka yoyote ya kuamua au kupitisha jambo bila kupata baraka za viongozi wa
Baraza la Uongozi Taifa kutoka kila chama.
“Kikao
hicho sijafahamu ajenda yake lakini ifahamike tu kwamba, ndani ya Ukawa kuna
vikao vitatu; kikao cha maofisa, kikao cha makatibu na kikao cha wenyeviti na
hufanyika kwa kuzingatia ratiba zake,” alisema na kuongeza:
“Kwa
hivyo utaratibu wa mgombea hauwezi kupatikana kwa sasa kwani hakuna chama
ambacho kimejadili ajenda yoyote au kupitisha majina ya wagombea wake.”
Sakaya
alisema kabla ya kujadiliwa ndani ya Ukawa, vikao vya mabaraza na kamati kuu za
vyama husika vitakuwa vimeshiriki kuchambua na kupitisha majina ya wagombea
wake wanaokidhi vigezo.
“Baada
ya hapo ndipo majina yatafikishwa Ukawa na kamati itachambua wanaoweza kusimama
kwa niaba ya Ukawa kutokana na tathimini yao watakayokuwa wameipata,” alisema
na kuongeza:
“Kwa
upande wa CUF, kalenda yetu inaonyesha kuwa na vikao mwishoni mwa mwezi huu.
Nadhani kutakuwa na mwelekeo juu ya uchaguzi ujao.” Viongozi wa juu wa Chadema
jana hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa Habari wake, Tumaini
Makene alisema kwa sasa chama hicho hakijafikiria kuwa na vikao vyenye ajenda
ya kuangalia jina litakalopitishwa kwa ajili ya kuingia Ukawa...
“Bado
kabisa kuhusu suala la kujadili mgombea urais wa Ukawa, hatujafikiria hilo ila
kinachotuumiza akili kwa sasa ni kero za daftari la wapigakura na kuwapo kwa
tume isiyokuwa huru ya uchaguzi. Ratiba ya ajenda hiyo ikitoka tutajulishana,”
alisema Makene.
Tweet