Benki Kuu ya Tanzania (BoT) |
WAFANYAKAZI
wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanaokabiliwa na tuhuma za kughushi
vyeti vya kidato cha nne wamekutwa wana kesi ya kujibu.
Uamuzi
huo ulitolewa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupitia ushahidi
wa mashahidi wanane wa upande wa mashtaka na kuona kwamba kuna haja kwa
washtakiwa kujitetea.
Washtakiwa
katika kesi hiyo ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth
Mahenge, Beata Massawe, Jackline Juma, Philimina Mtagurwa na Amina Mwinchumu.
Uamuzi
huo ulitolewa na Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, wakati kesi hiyo inaendeshwa
na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro.
“Mahakama
imepitia ushahidi wa mashahidi wanane wa upande wa Jamhuri, imeuona kwamba
ushahidi huo una nguvu, hivyo washtakiwa mna kesi ya kujibu, mnatakiwa
kujitetea,” alisema Hakimu
Mwaseba.
Baada
ya kusema hayo mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 17 na 18 mwaka
huu, kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.
Kwa
mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kughushi vyeti vya
kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao ambaye ni BoT.
Washtakiwa
Justina, Beata na Amina wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001. Christina,
Siamini, Janeth na Philimina, wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002.
Washtakiwa
hao wanadaiwa kughushi vyeti hivyo na kutoa hati za uongo BoT kuonyesha
vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania wakati si kweli.
Tweet