Raisi Kikwete alipozungumza na baadhi ya viongozi wa Dini |
Katika tamko la pamoja walilolitoa baada ya kukutana mjini Dodoma, viongozi hao (maaskofu) wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea
kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza
kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo
itakayolaumiwa.
Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile
la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa
Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Tamko
hilo la maneno 921, limeendelea kuwataka waumini wao kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma Katiba
Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya ‘hapana,’ msimamo
ambao tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyesema viongozi wa dini
hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya kura wanayostahili kupiga.
Pia,
Jukwaa hilo limewataka viongozi wakuu wa Serikali –Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
na Rais Kikwete wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini
waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu waliokutana nao si wawakilishi
rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au kukubaliana juu ya jambo la kitaifa.
“Maaskofu tuliokutana hapa (mjini Dodoma) hatuna hasira na
wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama
ambavyo wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na
sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga Taifa lenye umoja,
amani, utulivu na maelewano,” lilisema tamko hilo likihitimishwa kwa maneno ya
Biblia kutoka Mithali 29: 1, “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo,
atavunjika ghafla, wala hapati dawa.”
“Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao
utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa
Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu
za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri
Mkuu hazijajibiwa,” Ilieleza taarifa hiyo.
“Tunamtaka
Rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa utafiti
wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama
ya Kadhi. Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba
Serikali inajihusisha na itagharimia mahakama hiyo.”
Walisema;
“Yalijitokeza kwenye semina kwa wabunge mwishoni mwa wiki ni ishara ndogo ya
kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi yetu. Hapa tunajiuliza, endapo maneno
ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili kitu ambacho Serikali
haitajihusisha wala kukigharamia?”
Tamko
hilo lilionya: “Tunamtaka Rais (Kikwete) aiepushe nchi yetu na kuingizwa kwenye
mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa vigumu. Pia tunamwomba Rais
Kikwete akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na kinachotokea nchi ya Afrika
ya Kati, kati ya kundi la Seleka na kundi la Anti Balaka.
Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa Kamati
ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa
mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema
msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ni wa
hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
Rais Kikwete alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba
wanayoitaka wao... hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali
kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza,
imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au
kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete.
Nini maoni yako kuhusu hili swala? Washirikishe wengine habari hii.
Tweet