Jeshi
la Misri limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya Dola la Kiislamu
nchini Libya, baada ya kundi hilo kusambaza video mtandaoni inayoonyesha
Wakristo 21 kutoka Misri wakichinjwa.
Video
iliyosambazwa mtandaoni na Dola la Kiislamu inaonyesha Wamisri 21 wakiwa
wamevaa nguo za rangi ya chungwa na wakilazimishwa kupiga magoti ufukweni na
kisha wakiuliwa mmoja mmoja. Rais wa Misri, Abdel Fatah al-Sisi ameahidi
kuongeza nguvu katika kupambana na ugaidi. "Misri ina haki ya kulipiza
kisasi kwa wauajia na wahalifu hao ambao hawana utu kabisa. Tutaamua wenyewe
namna ya kulipiza kisasi na muda wa kufanya hivyo," amesema al-Sisi.
Jumatatu
ndege za kijeshi za Misri zilifanya mashambulizi ya angani katika maficho ya
Dola la Kiislamu nchini Libya nayo serikali ya al-Sisi imetangaza siku saba za
kuomboleza vifo vya Wakristo hao waliokuwa waumini wa madhehebu ya koptik.
Katika tamko lake uongozi wa kanisa la koptik umewataka waumini wake wawe na
imani kwamba nchi yao haitatulia hadi pale ambapo waliofanya uasi huu watapewa
adhabu wanayostahili.
Mwezi
uliopita tawi la Dola la Kiislamu nchini Libya lilikuwa limetangaza kuwa
limewateka nyara Wakristo 21 kutoka Misri na inaaminika kwamba hao ndio
wanaoonekana kwenye video hiyo.
Tangu
kuangushwa kwa utawala wa Muamar Gaddafi mwaka 2011 maelfu ya vibarua
wameelekea Libya kutafuta kazi na wengi wao wanatokea Misri. Hata hivyo
Wakristo wa koptik mara kwa mara wamelengwa na mashambulizi yaliyofanywa na
Waislamu wenye itikadi kali. Rais Abdel Fattah al-Sisi ameahidi kuhakikisha
usalama wa wananchi wake walioko Libya. "Nimeiomba serikali iendelee
kuwakataza Wamisri kusafiri kwenda Libya wakati huu mgumu ili kuokoa maisha
yetu. Nimezitaka pia taasisi husika zichukue hatua kuwawezesha Wamisri warudi
nchini mwao," alisema rais huyo.
Bunge
la Libya limetoa salamu za rambirambi na kuitaka jumuiya ya kimataifa iiunge
mkono Libya katika juhudi za kupambana na wanamgambo. Nao ujumbe wa Umoja wa
Mataifa nchini humo umewataka Walibya wote wakatae vitendo vya Dola la
Kiislamu. Rais Francois Hollande wa Ufaransa, ambaye alikuwa ameahidi kuiuzia
Misri ndege za kijeshi, ameelezea wasiwasi wake juu ya kukua kwa Dola la
Kiislamu.
Marekani
kwa upande wake imelaani mauaji ya watu hao 21. Msemaji wa ikulu ya White
House, Josh Earnest, amesema uovu wa Dola la Kiislamu usiojua mipaka
unaiunganisha jumuiya ya kimataifa katika kulipiga kundi hilo.
Tweet