Pambano la masumbwi linalosubiriwa na ulimwengu
mzima kati ya mabondia wawili bora katika miaka ya hivi karibuni Floyd
Mayweather na Manny Pacquiao linakaribia kutokea baada ya uthibitisho wa
mazungumzo ya pande mbili zinazowakilisha mabondia hao. Wakala wa Bondia
Mfilipino Pacquiao, Fred Sternburg amethibitisha kuwa mazungumzo baina ya kambi
za mabondia hawa wawili yanaendelea vizuri na huenda makubaliano yakafikiwa
siku sio nyingi. Wakala huyo hata hivyo amekanusha kuwepo kwa uthibitisho wa
tarehe ya mabondia hao kupanda ulingoni baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa wawili
hao watapambana Mei mbili mwaka huu. Pambano hili limewahi kuandaliwa kwa muda
mrefu bila mafanikio baada ya mabondia hawa kuonekana wakikwepana hususan Floyd
ambaye alikuwa akitoa visingizio vya kila aina ikiwemo kutaka mpinzani wake
apimwe vipimo vya dawa za kulevya. Taarifa zaidi zinasema kuwa mabondia hawa
wamekubaliana kugawana asilimia 60 kwa 40 ya mapato ya pambano hili ambapo
Floyd atachukua asilimia 60 na Manny atachukua asilimia 40.
Tweet