James Lembeli
James Lembeli, Mbunge wa Kahama aliyemaliza
muda wake amekataa kubadili msimamo wake wa kutogombea ubunge kupitia CCM
akisema atagombea nafasi hiyo kupitia chama kingine.
Akizungumza mjini hapa jana, Lembeli alisema
hawezi kubadili msimamo wake wa kuondoka CCM, kutokana na masharti mazito ya
kimila aliyopewa kabla ya kutangaza kuondoka katika chama hicho.
Baada ya uamuzi wake, watu mbalimbali, wakiwamo
maofisa wa Serikali na wafanyabiashara waliahidi kumsaidia hata nguvu ya
kifedha, wakimtaka atengue uamuzi wake achukue fomu katika Jimbo la Kahama
Mjini.
Alisema hawezi kukiuka masharti ya kimila kwa
kuwa yeye ni mtoto wa chifu. Mtoto huyo wa Chifu Daud Lembeli alisema kabla ya
kutoa uamuzi huo alikaa na mama yake mzazi, Maria Kalembo kuanzia saa 10 jioni
hadi saa nane usiku akizungumzia suala hilo hadi walipokubaliana.
Alisema baada ya mama yake kukubali na kutoa
baraka za kuhama CCM, alipigiwa ngoma za kimila za Waswezi, ambazo hutumika
kutoa baraka katika imani za kichifu akisema ndizo zilizohitimisha fursa za
kugombea kwake ubunge kupitia chama hicho.
“Najisikia amani kubwa kuondoka CCM, kabla
sijachukua uamuzi huu nilikuwa nikiishi kwa presha, hivi sasa nipo huru,
niacheni tu kama ni ubunge sikuzaliwa nao na unaweza kuishi bila ubunge na
maisha yakawa mazuri,” alisema Lembeli.
Tweet